The United Republic of Tanzania | Ministry of Information, Communication and Information Technology | ICT Commission
 INFORMATION AND COMMUNICATION TECHNOLOGY COMMISSION


Media Centre

Speech


Mheshimiwa Moshi Kakoso Mbunge - Chairperson of the Parliamentary Committee on Infrastructure

Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jerry Slaa, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Viongozi wote mlio Meza Kuu, na washiriki wa kongamano kwa ujumla.

Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa niaba ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Kamati ya Bunge ya Miundombinu, tunayo furaha kubwa sana kuungana na wewe leo hii kushuhudia kongamano hili la TEHAMA, linalofikia tamati. Mheshimiwa Waziri Mkuu, sisi kama Bunge ni mashahidi wa shughuli za Serikali ambazo Kamati ya Bunge ilipitisha bajeti yake. Tunaipongeza sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na jitihada za kipekee katika kufanya mapinduzi makubwa ndani ya sekta hii ya wizara ya TEHAMA.

Kuna mabadiliko makubwa sana ambayo yamefanywa na Serikali. Wizara hii hapo awali ilikuwa ikipokea fedha kidogo, lakini kwa dhamira thabiti ya Mheshimiwa Rais, kwa kipindi cha miaka mitatu (3) iliyopita, wizara hii imeongezewa fedha nyingi, na kuifanya kuwa moja ya wizara zilizovunja rekodi kwa kupata fedha nyingi. Matokeo ya uwekezaji huu yameanza kuonekana.

Taasisi nyingi zilizo chini ya Wizara ya TEHAMA zimepata mabadiliko makubwa, na tumeshuhudia karibu kila taasisi ikiwa na uwekezaji mkubwa kutoka Serikalini. Kwa upande wa Mkongo wa Taifa, mmefanya kazi nzuri sana. Tumepanga na kuongeza fedha ambazo zimeleta matokeo chanya, karibu kila kona tumeona upatikanaji wa huduma za mkongo huu, ambao sasa unafika hadi kwenye maeneo ya wilaya.

Ukitaka kufahamu umuhimu wa sekta hii, hitilafu ndogo kwenye mkongo wa Taifa husababisha madhara makubwa nchi nzima. Lakini tumeona jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita, kuhakikisha Posto Kodi zinafikishwa kwenye maeneo karibu kila sehemu. Ukienda vijijini, unashuhudia mabadiliko makubwa yaliyofanywa na Serikali. Mheshimiwa Waziri Mkuu, tuna sekta ya Mawasiliano kupitia TCRA, kuna uwekezaji mkubwa ambao sisi kama Bunge tumeona, na kuna mengi mengine yanayofanywa na Serikali. Bila juhudi hizi kubwa, tungekuwa na wakati mgumu sana!

Mheshimiwa Waziri Mkuu, namshukuru sana Waziri mwenye dhamana, kwa kazi kubwa ambayo anasimamia kwenye wizara hii. Anajitahidi sana katika utendaji wake, na leo hii, tunapozungumza, Mheshimiwa Waziri, kwenye kamati tuna mswada ambao upo Bungeni, na yeye anausimamia na kuusukuma ili uweze kusaidia taasisi zilizo chini ya wizara yake.

Tunaishukuru sana Serikali, na sisi kama Bunge, tunaahidi kuiunga mkono Serikali kwa sababu tunaona maendeleo makubwa yaliyofanywa na Serikali pamoja na dhamira yake. Wizara hii, ingawa wengine wanaweza kuiona kama wizara ndogo, imebeba karibu kila kitu ambacho Serikali inakitegemea. Tunakushukuru sana, Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa kushiriki nasi.

Asante sana!

Screenshot 2024-11-22 180854