The United Republic of Tanzania | Ministry of Information, Communication and Information Technology | ICT Commission
 INFORMATION AND COMMUNICATION TECHNOLOGY COMMISSION


Media Centre

Speech


Bwana Muhammed Hamis Abdula - Secretary General of the Ministry of ICT (Closing Speech)

Mheshimiwa Waziri wetu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Jerry William Slaa ambaye ni Mbunge, pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Mhandisi Marry Prisca Maundi.

Naomba kutambua uwepo wa kila mmoja wetu hapa kama tulivyotambulishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA. Naomba niwasalimu kwa jina la Muungano wa Tanzania… Kazi Iendelee!

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, kabla ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mungu wa Rehema, kwa kutuwezesha sote kukutana hapa leo asubuhi katika kongamano la TEHAMA la nane la mwaka 2024.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, kongamano hili ni la kipekee kwa sababu lina uwakilishi mkubwa wa mabalozi kutoka nchi mbalimbali. Hatukuwahi kuwa na kongamano lenye uwakilishi mzuri wa kimataifa kama huu wa mabalozi. Kwa mantiki hiyo, kongamano hili limepata sura ya kimataifa, ambapo washiriki kutoka ndani na nje ya nchi wameshiriki. Tutaweza kushuhudia katika kongamano hili utoaji wa Tuzo ya Kimataifa, ambapo Tanzania imepata heshima ya kuwa nchi ya kwanza kuwa mwenyeji wa mashindano yaliyoandaliwa na Umoja wa Afrika kuhusu masuala ya akili mnemba na roboti.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, tuzo hizo zitatolewa kesho kutwa ambapo mgeni rasmi atakuwa Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, lengo kuu la kongamano hili ni kuwakutanisha wadau wa sekta ya TEHAMA na kujadili masuala yanayohusu TEHAMA kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya TEHAMA nchini. Kwa kutambua umuhimu wa kongamano hili, kama tulivyoelezwa na Mkurugenzi Mkuu, litafanyika kwa siku tano. Tulianza na siku ya Wanawake na TEHAMA, tukaendelea na siku ya Vijana na TEHAMA jana, na leo hii unatufungulia rasmi kongamano hili. Hivyo, kongamano litaendelea hadi siku ya kufunga rasmi, kesho kutwa.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, kujumuishwa kwa makundi haya mbalimbali katika jamii, ikiwemo siku maalumu kwa ajili ya wanawake na vijana, kumetoa nafasi ya kujadili masuala yanayohusu teknolojia zinazoibukia.

Kaulimbiu ya kongamano hili ni Kutumia Uwezo wa Akili Mnemba na Roboti kwa Ajili ya Mapinduzi ya Kijamii na Kiuchumi.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, mada mbalimbali kama alivyoelezea Mkurugenzi Mkuu zimejadiliwa kuhusu matumizi ya akili bandia katika kutoa huduma mbalimbali kwenye sekta za afya, elimu, kilimo na kadhalika. Ndiyo uzuri wa kongamano hili, Mheshimiwa Mgeni Rasmi, ambapo tuna mada nyingi kutoka kwa watoa mada kutoka Marekani na Umoja wa Ulaya, na kwa hivyo, tuna sura nzima ya ulimwengu hapa.

Ni fursa kubwa tuliyoipata katika wiki hii ya siku tano kwa lengo la kujifunza na kuendelea kujifunza. Kama tunavyojua sote, dunia inaelekea kwenye teknolojia, hasa teknolojia zinazoibukia.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, wajibu wangu mkuu niliposimama hapa ni kukukaribisha wewe hasa. Nimeona ni vema nitoe maneno haya machache ya utangulizi kabla sijakukaribisha.

Basi, baada ya kusema hayo, sasa naomba kwa unyenyekevu kabisa nichukue fursa hii kukukaribisha wewe kuja kutoa hotuba ya ufunguzi wa kongamano hili la nane la TEHAMA.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, karibu sana!

11036A9884